Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO 
Kampuni ya Techno Net Scientific inayojishughulisha na uingizaji pamoja na uuzaji wa kemikali imekutwa na kemikali zilizoingizwa nchini kwa njia za udanganyifu kwa kutumia vibali vya bandia. 
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali(GCLA), Prof. Samwel Manyele alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampuni hiyo kukutwa na kemikali bashirifu bila kuwa na usajili wala kibali cha kufanya shughuli za kuuza na kusambaza bidhaa hiyo.
Prof. Manyele amesema kampuni hiyo ilikuwa na usajili wa miaka miwili kuanzia April 30 mwaka 2014 hadi Aprili 30, 2016 ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali kampuni hiyo ilipaswa kusitisha shughuli zake hadi pale cheti cha usajili kitakapopatikana.
“Ingawa shughuli zake zilisitishwa lakini kampuni hiyo iliendelea kufanya kazi bila kuwa na cheti cha usajili hivyo ofisi yangu iliungana na Mamlaka ya Kudhibiti dawa za kulevya na Mamlaka ya Chakula na Dawa kufanya ukaguzi wa pamoja ambapo kwa sasa tumewaachia vyombo vya dola kufanya uchunguzi wao” amesema Prof Manyele.
Amefafanua kuwa Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani Sura ya 182 na kanuni zake inatoa masharti kuwa kila mtu anayetaka kujihusisha na shughuli za kemikali kwa namna yoyote ni sharti awe amesajiliwa na kufanyiwa ukaguzi.
Aidha, ametoa rai kwa wafanyabiashara wote wa kemikali na umma kwa ujumla kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa makampuni na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu na wanaovunja matakwa ya Sheria katika uingizaji, usafirishaji, uhifadhi na utumiaji wa kemikali ikiwemo kemikali bashirifu nchini.
Prof. Manyele amewaomba wananchi kutoa taarifa na kuwafichua wafanyabiashara wa kemikali wanaokiuka matakwa ya Sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria ambazo zitapelekea wengine kuwa na matumizi salama ya kemikali na kuzuia madhara kwa watu na mazingira.
 Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Profesa Samwel Manyele (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu kampuni ya TECHNO NET SCIENTIFIC kukutwa na kemikali bashirifu bila kuwa na usajili wala kibali cha kufanya shughuli za kuuza na kusambaza kemikali. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma za Ubora wa Bidhaa, Bw. Daniel Ndiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara Bw. George Kasinga na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba.  Bi. Hadija Mwema, 
Sehemu ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Profesa Samwel Manyele (hayupo pichani) leo Jijini Dar es Salaam uliohusu kampuni ya TECHNO NET SCIENTIFIC kukutwa na kemikali bashirifu bila kuwa na usajili wala kibali cha kufanya shughuli za kuuza na kusambaza kemikali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...