Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu
Bw. Eric Shitindi (aliyesimama) akizungumza na wadau kutoka Asasi mbalimbali
zinazojishughulisha na masuala ya vijana alipokua akifungua kikao cha kupitia
mwongozo wa Stadi za Maisha wa mwaka 2009 kwa vijana walio nje ya shule
leo Jijini Dar es Salaam.
Na Genofeva Matemu - Maelezo
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu
imewakutanisha wadau mbalimbali kutoka Asasi zinazojishughulisha na masuala
ya vijana ili ziweze kushirikiana na serikali kupitia na kuboresha Mwongozo
Sanifu wa Stadi za Maisha kwa Vijana kwa kubadilishana uzoefu walionao na
kuuwezesha mwongozo huo kumsaidia kijana katika mazingira ya sasa.
Akifungua kikao cha wadau hao Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana,
Ajira na wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi amesema kuwa msingi mkubwa wa
kuboresha mwongozi sanifu wa stadi za maisha kwa vijana ni pamoja na
kuangalia namna gani serikali inaweza kuwasaidia vijana kwa kuwawezesha
kujitambua, kujiendeleza wenyewe na kukuza uchumi wa nchi yetu.
"Mwongozo wa stadi za maisha umekua ukiwajenga vijana kwa kuwaandaa
kujitambua ili waweze kuhimili changamoto mbalimbali zilizopo kama vile
vishawishi mbalimbali vinavyowakabili, magonjwa, matumizi ya madawa ya
kulevya, mimba za utotoni pamoja na ukosefu wa ajira" amesema Bw. Shitindi
kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi
amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi, kisayansi na
kijamii serikali imeona ni vyema kukaa pamoja na wadau hao kuangalia yale
yaliyomo kwenye Mwongozo wa mwaka 2009 na kufanya uchambuzi yakinifu
kwa kila eneo ndani ya mwongozo huo.
aidha Bw. Kajugusi amewashukuru wadau kutoka Asasi mbalimbali
zinazojishughulisha na masuala ya vijana kwa kuisaidia serikali kufikisha elimu
ya stadi za maisha kwa vijana kulingana na mipango na programu zao na
kuwahaidi kuendelea kufanya nao kazi katika kujenga taifa lenye vijana
wanaojitambua.
Naye Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Shirika la Kimataifa la Idadi ya watu
Bibi. Tausi Hassan ameishukuru serikali kuwakutanisha wadau wanaofanya kazi
na vijana moja kwa moja kushirikiana katika kuboresha Mwongozo wa Stadi za
Maisha kwa vijana kwani ushirikiano huo utalenga nyanja zote hivyo kupata
mwongozo unaokidhi matakwa ya vijana kitaifa.
Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi (katikati)
akifafanua jambo wakati wa kikao na wadau kutoka Asasi mbalimbali
zinazojishughulisha na masuala ya vijana kupitia mwongozo wa Stadi za Maisha
wa mwaka 2009 kwa vijana walio nje ya shule leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi Ushauri Nasaha Bw. Juma Mswadiku (kushoto) akitoa
hoja wakati wa kikao na wadau kutoka Asasi mbalimbali zinazojishughulisha na
masuala ya vijana kupitia mwongozo wa Stadi za Maisha wa mwaka 2009 kwa
vijana walio nje ya shule leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha kupitia mwongozo wa Stadi za Maisha
wa mwaka 2009 kwa vijana walio nje ya shule wakifuatilia mada zilizokua
zikiendela leo wakati wa kikao na wadau kutoka Asasi mbalimbali
zinazojishughulisha na masuala ya vijana.
Mwezeshaji kutoka Chama cha Stadi za Maisha (LISA) Bw. Elemeth Oloo
akitoa mada kwa wadau kutoka Asasi mbalimbali zinazojishughulisha na
masuala ya vijana wakati wa kikao cha kupitia mwongozo wa Stadi za Maisha
wa mwaka 2009 kwa vijana walio nje ya shule leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na: Genofeva Matemu - Maelezo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...